Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametoa maagizo
kwa viongozi wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate kuhakikisha wanatatua
migogoro na wafanyakazi pamoja na kusimamia haki zao ipasavyo.
Waziri Mhagama ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake Wilayani
Same alipofanya ziara katika Shamba la Hassan Sisal Estate ikiwa ni utekelezaji
wa maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi
aliyoyatoa Julai 20, 2019 alipotembelea shamba hilo lililopo Mkoani
Kilimanjaro, Wilaya ya Same.
Akizungumza na wafanyakazi pamoja na viongozi wa shamba hilo,
ameeleza kuwa waajiri wanatakiwa kutekeleza matakwa yote kwa mujibu wa Sheria za ajira na mahusiano kazini kwa
kuzingatia miongozo na kanuni ambayo inasimamia haki,usawa na misingi thabiti kwa
wafanyakazi.
“Tunataka kuona ninyi kama waajiri mnakuwa na vikao vyenye tija
na wafanyakazi katika kuleta suluhu ya masuala mbalimbali ya kazi mnatumia njia
zilizo halali kuwapatia haki wafanyakazi wenu,” amesema Mhagama
Katika hatua hiyo Mhagama amezitaka kampuni mbili zilizopo
katika shamba hilo yaani Unique Consultancy na UPAMI kuhakikisha wanatoa huduma
bora kwa wafanyakazi hao, ikiwemo kuwasilisha michango yao kwa wakati kwenye
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF) ikiwemo kuweka wazi mikataba yao.
“Malalamiko na
Manung’uniko ya wafanyakazi hawa ni mengi, mnatakiwa mnapaswa n kuyajadili kwa na mkubaliane kwa pamoja namna
bora ya kutatua matatizo yanayowakabili na
yatakayojitokeza hususani kwenye mikataba,” amesema Mhagama.
Katika hatua hiyo, Mhe. Mhagama alimuagiza Meneja wa Wakala wa
Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA), kufanya kanguzi za mara kwa mara katika
shamba hilo na kuangalia kama wafanyakazi wanakabidhiwa vifaa vya kujinginga na
madhara kazini (Protective gears) kwa wakati, pamoja na kusimamia zoezi la
upimaji afya kwa wafanyakazi hao.
Akitoa maelekezo kwa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF) Mkoa wa Kilimanjaro, amemtaka kukabidhi kadi za uwanachama kwa
wafanyakazi wa shamba hilo na kufuatilia uwasilishaji wa michango yao kutoka
kwa waajiri wao.
Sambamba na hilo, Waziri Mhagama ametaka Afisa Kazi
Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea shamba hilo na maeneo mengine
mbalimbali katika mkoa huo ili kuelimisha wafanyakazi sheria mbalimbali za kazi
na ajira zitakazo wawezesha kutambua haki zao za msingi.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa maelekezo juu ya uwepo wa vyama vya
wafanyakazi kwenye mashamba yote ya katani yaliyopo nchini, vitakavyosadia
kuongeza tija na ufanisi katika shughuli mbalimbali za utendaji kazi.
Pamoja na hayo, Mheshimiwa Mhagama amewataka viongozi wa shamba
hilo kuendelea kusimamia vizuri maslahi ya wafanyakazi ili waweze kuleta tija itakayowapa fursa
katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku wanapokua kazini.
Naye, Meneja Mshauri wa Shamba hilo, Bw. Ndekirwa Nnyari ameahidi
kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo kuwa na majadiliano ya mara kwa
mara na wafanyakazi kwa itakayowapa munufaa ya pamoja.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF),
Bw. Victor Luvena amesema kuwa watatekeleza maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa
Waziri kwa kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaoshindwa kutekeleza.
Hata hivyo mmoja wa Wafanyakazi wa Shamba hilo, Bi. Cheshi Juma
amesema kuwa ujio wa Waziri na wataalamu alioambatana nao utasaidia kuondoa
kero za wafanyakazi na kujenga mahusiano mazuri na waajiri wao.
“Tumehamasika sana kuona Serikali yetu ipo pamoja nasi katika
kutetea maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kero tulizokuwa tukikabiliana nazo
katika maeneo ya kazi,” amesema Cheshi.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni