Rais Uhuru Kenyatta amemteua Joseph Nkaissery kuwa waziri mpya wa mambo ya ndani na kumfuta kazi mkuu wa polisi, kufuatia mashambulizi mengine yaliyogharimu maisha ya watu 36 usiku wa kuamkia leo. Akizungumza na wanahabari mchana wa leo, Rais Kenyatta amesema nchi yake itaendelea na mapambano yake dhidi ya makundi ya siasa kali, licha ya kukabiliwa na hali ngumu. Kenyatta amewatolea wito Wakenya kujipambanua na makundi hayo na kuunga mkono vita dhidi ya ugaidi. "Wapendwa Wakenya, muda umesika wa kila mmoja wetu kuamua na kuchagua ama kusimama upande wa Kenya ya kidemokrasia, yenye uhuru na uwazi, inayoheshimu utawala wa sheria, uhai, na uhuru wa kuabudu, au kusimama upande wa wenye siasa kali, ambao ni wakandamizaji, wasio uvumilivu na wauaji." Mapema, kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la al-Shabaab nchini Somalia, lilidai kuhusika na mauaji hayo ya watu 36 katika Kaunti ya Mandera, kaskazini mwa Kenya. Watu wenye silaha wanaripotiwa kulivamia eneo la wachimba mawe, ambapo waliwatenganisha Waislamu na wasiokuwa Waislamu kisha wakaanza kuwapiga risasi wasiokuwa Waislamu, mfano wa mashambulizi ya wiki iliyopita dhidi ya basi moja la abiria kutokea huko huko Mandera. Mashambulizi ya jana yalifanyika saa moja tu baada ya hoteli moja mjini Wajir, pia iliyo kaskazini mwa Kenya, kushambuliwa kwa guruneti na mtu mmoja kuuawa na wengine 13 kujeruhiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni