![]() |
Halimashauri ya Wilaya ya moshi mkoani Kilimanjaro
imeanzisha kampeni mpya ambayo itasaidia kudhibiti uhifadhi wa mazingira kupitia shughuli zinazofanywa na binadamu na kuchangia uharibifu wa mazingira
hususani kwa wafugaji wanaoachia mifugo yao ovyo inayoharibu miche ya miti
inayoendelea kupandwa na serikali na wadau wa mazingira wilayani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi ,Angelina Marko ambaye ni katibu tawala wa wilaya hiyo wakati wa ghafla ya uzinduzi
wa zoezi la upandaji miti wilaya humo katika shule ya msingi Mabungo kata ya kirua
kusini moshi vijijini amesema utunzaji wa miti ni zoezi endelevu ambalo kila
mwananchi anapaswa kuhakikisha anaunga mkono jitihada muhimu zinazofanywa na Serikali
na wadau wa mazingira katika kulinda uoto wa asili.
“Haiwezekani
serikali na wadau wa mazingira waweke jitihada za kupanda miti hatimaye mifugo
ije nakuharibu ,watachukuliwa hatua watakao achia mifugo yao itakayosababisha
uharibifu wa miti inayopandwa, zipo sheria zilizowekwa za vijiji na wilaya
katika kudhibiti mifugo itakayosababisha uhariifu wa mazingira.”alisema
Akifafanua zaidi amesema kampeni hiyo imeanzishwa kwa tija ili kukamata mifugo ambayo itakua
inazurura ovyo na kusababisha uharibifu wa miche ya miti inayoendelea kupandwa
wilayani katika maeneo mbalimbali Wilayani humo,ambapo mnyama yeyote atakayekamatwa atatozwa fine
ama kupelekwa mnadani ili kukomesha uharibifu huo.
Akizungumzia kuhusu hali halisi ya mazingira kwa sasa amesema imebadilika
kutokana na kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na imepelekea kupungua kwa
theluji ya Mlima Kilimanjaro ambapo wataalamu wanasema imebakia 18.2% jambo
ambalo linaweza kusababisha kupungua kwa soko la utalii wa watalii watakaotembelea mlima huo.
“Tumekua tukifanya jitihada hizi za kupanda miti maeneo
mbalimbali ya wilaya yetu tangu mwaka( 2014) hadi sasa (2019) lakini je
ufuatiliaji unakuaje baada ya kupanda miti hii ,ningetoa hamasa kwa viongozi wenzangu
na wadau wa mazingira tuwe tunahakiki miti tunayoipanda na kutembelea kila baada
ya muda ili kujua maendeleo.”alisema Angelina
ambaye pia amechangia miche ya miti 500.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi
walishiriki zoezi hilo la upandaji miti katika eneo la shule ya
Mabungo,wamesema wanaunga mkono jitihada za Serikali katika kupanda na
,kulinda mazingira kwani miti hiyo
inafaida mbalimbali kama kuwaletea mvua
pamoja na hewa nzuri .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halimashauri hiyo Bw. Michael Kilawila amesema upandaji wa miti ni njia mojawapo ya utunzaji mazingira kwa
lengo la kulinda uoto wa asili pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia
nchi yanayoweza kujitokeza endapo uharibifu wa mazingira utatokea na kujinasibu na baa la njaa .
“Baadhi ya wananchi hawafahamu umuhimu wa miti,
lakini ukweli ni kwamba miti hii ni lulu ambayo tunapaswa kuilinda kwani sisi
tunaitegemea hewa tunayoivuta inatokana na miti hii sambamba na kuleta unyevu katika mimea tunayoiotesha.”alisema Kilawila
Akisoma taarifa ya upandaji miti wilaya ,Afisa
misitu wa wilaya hiyo ya Moshi,Joshua Mungure amesema halimashauri hiyo imekua ikipanda
miti kila mwaka hususani kipindi vya mvua za masika na vuli kwa lengo la
kuhamasisha wananchi na wadau kutumia mvua zinazazoendelea kunyesha kupanda miti.
Amesema licha ya kuwepo kwa mafanikio katika
upandaji miti bado kuna changamoto kwa
baadhi ya wananchi wasio na uelewa juu ya utunzaji wa mazingira,ambao
hukata miti ovyo maeneo ya misitu ,ulishaji na uchungaji wa mifugo maeneo ya
hifadhi na tambarare na kwamba utatuzi wa changamoto hizo elimu imeendelea
kutolewa kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kuepusha uharibifu huo.
Hata hivyo kwa upande wake mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya msingi
Mabungo iliyofanyika uzinduzi huo wa kupanda miche hiyo Bw. Robert Materu amesema imepandwa
miti 320 katika eneo la wazi la shule hiyo huku akishukuru uongozi wa wilaya kwa kufanya uzinduzi huo
shuleni hapo na kwamba watailinda miti hiyo ili iweze kukua na kustawi.
Halimashauri hiyo ya Moshi imeanza zoezi hilo kwa
kuanza kupanda miti 320 katika shule hiyo kati ya miti 1000 iliyokua inatakiwa
kupandwa ambapo wilaya hiyo kwa mwaka huu inatarajia kupanda 9000 maeneo
mbalimbali yanayozunguka mlima Kilimanjaro.
