Tafuta katika Blogu Hii
Alhamisi, 19 Oktoba 2017
MAKAMU WA RAIS MH.SAMIA HASSAN AMESISTIZA UTII WA SHERIA BILA SHURUTI NA UWAJIBIKAJI KWA VYOMBO VYENYE DHAMANA KATIKA KUTEKELEZA WAJIBU WAO.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaonya askari wa kikosi cha usalama barabarani kutogeuza tochi kuwa chanzo cha kudai rushwa sambamba na kutowanyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani uliofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi amesema takriban asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu kutokana na utumiaji wa simu wakati wa kuendesha gari, uchovu wa madereva na ulevi.
Samia amesema sababu nyingine zinazochangia ajali za barabarani ni miundombinu mibovu ya barabara inayochangia kwa asilimia nane na ubovu wa magari unaochangia kwa asilimia 16 huku idadi kubwa ya ajali hizo zinasababishwa na uzembe wa waendesha bodaboda ambao unaweza kuepukika na kuokoa maisha ya wengi.
Akizungumzia athari za ajali hizo Samia amesema Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane kutokana na uzembe wa madereva wachache wasiokua na uzalendo wa kutii sheria bila shuruti.
Akitoa idadi ya takwibu kitaifa makamu wa rais amesema“Mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwa na ajali za pikipiki 42,721 zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597,” .
Akizungumzia hali hiyo kwa Mkoa wa Kilimanjaro amesema “mkoa umeripotiwa kuwa na ajali 84 za bodaboda zilizosababisha vifo 61 na majeruhi 21”.
Katika hatua hiyo ameeleza kusikitishwa kwa Tanzania kutajwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni nchi inayoongoza kwa ajali ikiwa na asilimia 33.
Ambapo amelazimika kuliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau kuzingatia na kuelekeza nguvu kwenye kudhibiti makosa makubwa matano hatarishi.
Ameyataja makosa hayo kuwa ni mwendo kasi, ulevi, kutovaa kofia ngumu, kutovaa mikanda ya usalama katika gari na ukosefu wa vifaa vya usalama kuwalinda watoto wadogo wakiwa ndani ya gari.
Makamu wa Rais amewataka kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wote kupitia taasisi mbalimbali, kujipanga na kuhakikisha wanabadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na tatizo la ajali.
Amewataka kutoa machapisho yenye kutoa elimu kwa makundi yote ya watumiaji wa barabara na kusimamia mafunzo ya umahiri wa uendeshaji wa vyombo vya moto.
Pia, amewataka askari wa usalama barabarani kufanya doria za mara kwa mara katika barabara kuu na za ndani ili kudhibiti makosa ya usalama barabarani na ajali zisizo za lazima.
Kwa upande wa abiria amewataka kuwa makini na kujenga tabia ya kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni