Tafuta katika Blogu Hii

Jumatatu, 25 Februari 2019

MVUA YAKWAMISHA MTANANGE SERENGETI BOYS DHIDI YA POLISI TANZANIA .

Kocha Oscar Milambo akiwafunda wachezaji wake klabu ya mchezo dhidi ya Polisi Kilimanjaro
 Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) Serengeti Boys imeshindwa kucheza mtanange wake wa kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania ya mjini Moshi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo. 

Mtanange ambao ulikuwa muhimu kwa timu zote mbili ulichezwa kwa dakika 12 tu baada ya mvua kuanza kunyesha hivyo kusababisha uwanja wa Ushirika mjini Moshi kujaa maji kwa kiwango ambacho kisiweza mpira kuchezwa. 

Akizungumza na vyombo vya habari Kocha Oscar Milambo wa Serengeti Boys amesema waliona ni vema kusitisha mechi hiyo kutokana na kujali usalama wa wachezaji wake endapo wangeendelea kucheza. “Unajua mchezaji anapocheza kwenye maji au utelezi anaweza kuanguka na kuvunjika hata pasipo kuchezewa rafu. 

Halafu pia tuna mashindano makubwa mbeleni ambayo bado tunawahitaji vijana wetu wawe kwenye ubora pasipo majeruhi yoyote,” alisema Milambo. Serengeti Boys inayojiandaa na mashindano ya Afrika kwa vijana U-17 ambayo Tanzania ndiyo mwenyeji imeweka kambi yake jijini Arusha. 

Mashindano hayo ya Afrika yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili mwaka huu jijini Dar es Salaam huku Tanzania ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri ili kushiriki mashindano ya dunia nchini Peru baadaye mwaka huu. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania Ami Ninje aliwashukuru wakazi wa Moshi na Kilimanjaro kwa ujumla waliojitokeza kushuhudia mtanange huo. Aidha Ninje aliongeza kuwa wana siku chache za kukaa Tanzania kwani safari ya kwenda nchini Uturuki kwa kambi ya siku 10 imewadia. 


“Machi Mosi tutakuwa safari kuelekea Uturuki katika mji wa Antalya ambako timu zote washiriki wa AFCON U-17 tutakuwa huko kwa kambi ya siku 10 kujiandaa na mashindano lakini kubwa zaidi kwa vijana wetu ni kuona vijana wenzao hususani barani Ulaya wanachezaje mpira wa kisasa,” alisema Ninje.
TIZAMA PICHA HIZI KATIKA UWANJA WA CHUO KIKUU CHA USHIRIKA MOSHI.
Waamuzi wa mchezo wa kirafiki baina ya Polisi Kilimanjaro na Serengeti Boys
Kikosi cha kwanza cha Serengeti Boys kilichoanza dhidi ya Polisi Kilimanjaro katika uwanja wa Ushirika Moshi, Kilimanjaro.
Hekaheka uwanjani kabla ya mvua dakika tano tu baada ya mchezo kuanza.
Mvua iliyokwamisha mchezapo wa kirafiki baina ya Polisi Tanzania na Serengeti Boys Februari 25 mwaka huu.
Kocha Emmanuel Amunike wa timu ya Taifa Stars akibadilisha mawazo katika mchezo wa kirafiki baina ya Polisi Tanzania na Serengeti Boys ulichezwa kwa dakika 12 tu kwenye uwanja wa Ushirika mjini Moshi kabla ya kusimamishwa kutokana na mvua. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni