Tafuta katika Blogu Hii

Jumatatu, 8 Aprili 2019

MAKALA ;TANZANIA BILA MADAWA YA KULEVYA INAWEZEKANA ! JE,MIKONO YAKO IPO SALAMA?


 

Msiwaone wamebeba mabegi mkazani ni wasafiri au wanafunzi mitihani yao ni kupenya katika viunga mbalimbali vya miji kutimiza azima zao.
Kwa miaka mingi hivi sasa biashara ya madawa ya kulevya imekua ikishamiri siku hadi siku kama biashara nyingine zinazofanywa na wajasiriamali tofatoutitofauti na kusababisha madhara mbalimbali  kwa watumiaji ,wanajamii , taifa la leo na la kesho licha ya kuwepo kwa sheria ya mwaka 2015 kifungu namba 5 inayopinga matumizi na biashara hii haramu.
Mbali na kuwepo kauli mbiu inayosadifu mwenendo utakaokuza uchumi wa kati na sera ya taifa la Tanzania “HAPA KAZI TU”serikali lazima ichukukue hatua thabiti yakukomesha na kutokomeza aina mbalimbali za madawa ya kulevya yanayopatikana hapa nchini ikiwemo bangi,kokeini,miadarati na nyinginezo.
Sina budi kusema serikali yaani mimi ,wewe na viongozi mbalimbali tuliowapa dhamana ya kutuongoza bila kuwasahau  wazalendo wote wenye mapenzi  mema na taifa lao haijalishi ni mjini au vijini kwani waswahili husema “maji ukishayavulia nguo sharti uyaoge” halikadhalika “Tembo hashindwi na mkonga wake” kwa mantiki hii  tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kufikia malengo ya kukomesha na kutokomeza kabisa matumizi ya madawa ya kulevya.
Mashirika mbalimbali na taasisi za kidini zimekua zikipambana vilivyo kuwaelimisha waumini wa kada mbalimbali kupitia mahubiri na makongamano juu ya hathari zinazopatikana na matumizi hayo huku ushirikiano hafifu katika kuwabaini wahusika  kutoka kwa  wananchi, mamlaka husika zilizopewa dhamana ya kushughulikia maswala haya nyeti na  baadhi ya viongozi tuliowapa ridhaa ya kutuongoza wakituhumiwa kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuendeleza biashara hii haramu kwa mantiki ya kupalilia na kulinda kura  na nyanzifa zao katika kipindi kijacho.
Hii ni dhairi kwamba viongozi hawa wanawafahamu fika baadhi ya wafanya biashara hao katika maeneo yao  na kama sio kuwafahamu fika, wanatambua uwepo wa biashara hizi  katika maeneo mbalimbali wanayoyasimamia katika shughuli zao za kiutawala.
Vimekuepo viashiria mbalimbali vya upatikanaji wa madawa hayo ya kulevya kama uwepo wa viatu juu ya  nyaya za nguzo za umeme,mifuniko ya ndoo na kadhalika huku ushindani wa soko ukisimamiwa na wananchi wa  tabaka la chini.
Nchini Tanzania baadhi ya viongozi wamekua wanatumia fulsa hii kwa wananchi kama mtaji wao wa kisiasa katika kampeni mbalimbali wakiwa na lugha iliosheheni ladha nzuri ya sera na mikakati ya kimaendeleo katika miundombinu mbalimbali ikiwemo Afya ,Elimu nk. lakini sio kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa  biashara hizi haramu.
Ukipita katikati ya miji utaliona taifa la leo likiwa limegubikwa na ulevi wa madawa hayo,utayaona na hata kukutana na makundi mbalimbali ya watumiaji na waathiriwa wa dawa hizo wakijaribu kupambambana kwa kila hali kupata chochote wakijidai wapiga debe na wabeba mizigo ndani ya miavuli iliyosheheni maasi mbalimbali ikiwemo udokozi,wizi,ubakaji na hata ulawiti.
Sauti zao zinasikika katika ladha tofautitofauti zikiwa zimebeba fikra chanya za uwajibikaji “mia tano mpaka nitakapoufikisha mzigo” kauli hii inachukua hatamu “mjini hakuna mashamba karibu tuwajibike hatuwezi kulima lami”hapo inakubidi uwe makini kuchunga vile ulivyo navyo haijalishi ni mkate,simu ya mkoni,fedha,pochi au chochote ulichobeba kama zawadi huko uendapo.
Swali la kuweza kujiuliza je?katika maeneo hayo ni kwamba hakuna uongozi au viongozi hao ni vipofu wa fikra au wapo katika miavuli ya kulinda kura zao kupitia chaguzi mbalimbali.
Jibu la haraka linaweza kupatikana katika fikra hii “bora liende matumizi ya kwao ,waathirika wao kura za kwangu” na kuibua sura yenye taswira tofauti kwa viongozi wateule wa Mh.Rais kuwa wana viburi hawafai kuwa viongozi na kufikia hata hatua ya udhalilishaji na kuingiliwa faragha zao.
Ili kuendana na kasi ya Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli “Tanzania ya viwanda”ni vyema wateule wa rais kuunda jukwaa la pamoja na kuungana kwa pamoja katika kukomesha biashara haramu kwa kushirikiana na vyombo vya dola ambapo kimsingi vyombo hivyo wanadhamana kubwa ya kulinda rasilimali mali na watu kwani wao ni Wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama.
Ninaposema rasilimali watu ninamaanisha kwa dhati kabisa viwanda bila nguvu kazi watu ni kazi bure kutokana na athari mbalimbali zinazowakuta walengwa ikiwemo sababu za kiafya na kiuchumi.
Hii ni dhairi kwamba waraibu wengi wa dawa za kulevya wanaopatikana mtaani niwaaathirika wa virusi vya ukimwi (VVU)asilimia kubwa wamekua  wakijikatia tamaa huku wauzaji wakijipatia faida kedekede “wanaishi vizuri ,wanamiliki vitega uchumi vya gharama kubwa ikiwemo magari ya kifahari na majumba”.
Mimi nafikiri mkono mrefu wa serikali ungeanza kuwakamata na kuwachukuli hatua stahiki tungeweza kumaliza tatizo hili kabisa, mawakala na wasambazaji wa dawa hizi za kulevya  ndio chazo cha kushamiri kwa biashara hii hivyo,wakiwaunganishwa na watumiaji kunaweza kupatikana suluhu na kuifanya Tanzania ya Viwanda na  bila madawa inawezekana kwani wote hawa jamii inawatambua.
Mchambuzi wa makala hii anaweza kuwa na mwarobaini sahihi wa tatizo hili kama haki itatendeka kwa usawa na sio kununuliwa inasikitisha kabisa kuona biashara hii inafanyika kwa uwazi kabisa kama biashara halali”wauzaji na wasambazaji wamekua kama wamachinga katikati ya mji na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wakishindwa kutimiza wajibu wanawakamata sasa hivi baada ya muda wamewaachia kwa mantiki hii baadhi yao wamekua kama watoza ushuru“je? tupo salama!
Kumekuwepo na viongozi wenye ujasiri na utashi mkubwa wakudhibiti maovu kwa kauli mbiu mbalimbali kama “watapata tabu sana,Dar es salaam salama”na kadhalika huku wakiibua hisia zenye tija kwa baadhi ya watanzania wenye nia salama na nchi yao hii inaonyesha dhahiri kwamba Mh.Rais ana nia njema yakuifikisha Tanzania mbali kiuchumi “HAPA KAZI TU.”
Mchambuzi wa makala hii hana budi kusema huenda chanzo cha kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya nchini Tanzania inatokana na kutokuwepo kwa viongozi wasio wazalendo na uwepo wa baadhi ya  nchi jirani  kuhalalisha matumizi ya madawa ya kulevya kama moja ya starehe na faragha ya mtu hivyo kurahisisha upatikanaji huo na kuleta taswira yenye uhalisia wa biashara hiyo kuanzia mipakani mwa nchi hizo kuelekea vijijini ,mjini,kata,tarafa, wilaya,mkoa na hatimaye nchi nzima hivyo kuitaka serikali kutizama swala hili kwa jicho la tatu na kuleta fikra mpya.