Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt.Anna Mgwhira amewataka viongozi wa serikali Mkoani humo kujikita zaidi katika kusimamia miradi ya maendeleo katika ngazi ya Vijiji, Kata,Tarafa na Wilaya hali itakayoleta tija kwa wanachi katika kuzifikia huduma muhimu.
Kiongozi huyo ametoa rai hiyo kufuatia ziara yake ya siku moja iliyolenga kukagua miradi ya ujenzi wa hospitali katika wilaya ya Rombo na Siha mkoani humo ambapo ameonyesha kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizofikiwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
Akifafanua zaidi Dkt.Mghwira amesema hatua mbalimbali za ujenzi huo zinatokana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza ilani yake kwa vitendo katika kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana katika ngazi ya vijiji,Kata,Tarafa na Wilaya na kuwataka wananchi kuipokea miradi hiyo ambayo imelenga kuwasaidia na kuboresha mfumo wa Afya kwa walengwa.
Katika hatua hiyo Mgwhira amezitaka mamlaka zilizopewa dhamana ya
kusimamia ujenzi wa majengo ya hospitali ya Siha kuongeza kasi kiutendaji katika kuhakikisha wanakamilisha
ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa na kuwaondolea adha wananchi kuzifikia huduma muhimu za kitabibu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Rombo Bi.Agnes
Hokororo amesema ujenzi wa Hospitali hiyo inayojengwa kwenye kata ya Kirongo Samanga, Kijiji cha Kiwanda Mteri itasaidia wakazi wa eneo hilo sambamba na kuimarisha
miundombinu mbalimbali ikiwemo Barabara,Maji na Umeme.
Bw. Frimini Peter ni mmoja wa wakazi wa eneo
hilo ambalo linajengwa hospitali hiyo amesema ni matumaini yao kwamba ujenzi
huo ukikamilika utawasaidia kwa kiasi kikubwa na kuwanufaisha kwani wamekua wakizifuata huduma za afya kwa umbali mrefu ,hali inayosababisha wakati mwingine wagonjwa kufia ndani au njiani kwa kukosa uwezo wa kuwafikisha hospitalini.
Ujenzi huo wa hospitali hizo mbili Rombo na Siha
kuanza kwake hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi billion 3 za kitanzania
zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya kwenye wilaya
hizo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi june mwaka huu.Katika Picha hawa ni Mafundi wakitimiza majukumu yao. |
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt.Anna Mgwhira akishauri jambo kuhusiana na eneo linaloonekana katika moja ya Msingi wa jengo linalotazamiwa kujengwa na kukamilika siku za usoni katika wilaya ya Rombo. |
Aliyenyoosha mkono ni Afisa Mipango Miji wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw.Godbless Kimaro akishauri jambo kuhusiana na ujenzi huo. |