Kundi la watu wanaoaminika kuwa ni majambazi
wakiwa na silaha za moto na mapanga, wamevamia watalii 17 kutoka mataifa
mbalimbali na kuwapora kiasi kikubwa cha fedha, kamera na kompyuta mpakato
(Laptop), kisha kuwajeruhi wanne na kutoweka.
Tukio hilo kubwa kuwahi kutokea siku za hivi
karibuni mkoani Kilimanjaro, limetokea juzi alfajiri eneo la Mailisita kwenye
hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge inayomilikiwa na mfanyabiashara
Cuthbert Swai, ambaye pia anamiliki kampuni ya wakala wa utalii ya Ahsante
Tours ya mjini hapa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, watalii
hao kutoka mataifa mbalimbali, walikumbwa na mkasa huo wakiwa wamelala ndani ya
mahema majira ya saa 9 alfajiri, ambako walitishwa kwa bunduki na mapanga kabla
ya kuporwa mali zao.
Katika tukio hilo, watalii watatu waliporwa zaidi
ya dola 2,090 za Marekani, mmoja pauni 110 za Uingereza na euro kiasi
kisichojulikana, sh milioni 5.4, kamera zaidi ya nne na moja ikiwa na thamani
ya sh milioni 1.5 na nyingine ikiwa na thamani ya dola 3,000 za Marekani, zaidi
ya sh milioni 4.5.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizothibitishwa
na Kamanda wa Mkoa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Robert
Boaz, majambazi hao kabla ya kufanya uhalifu huo, waliwakusanya watalii hao
eneo moja na kuanza kuwapora kila kitu walichokuwa nacho.
Hata hivyo, Kamanda Boaz hakuweza kulizungumzia
tukio hilo kwa kina, ikiwamo kutaja majina ya watalii hao, uraia wao na thamani
halisi ya mali walizoporwa, kutokana na kuwa katika pilikapilika za kwenda
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kupokea ugeni wa Spika wa
Bunge la Nigeria.
Kamanda Boaz, aliwaambia waandishi wa habari
waliofika ofisini kwake jana kuwa tukio hilo atalitolea maelezo kamili leo
kutokana na kutingwa na ugeni huo.
Ofisa mmoja wa polisi aliyeomba kutotajwa jina
lake, alisema kuwa miongoni mwa watalii hao walioporwa mali zao, wako wanne
waliokuwa wakijiandaa kuondoka na ndege alfajiri hiyo kupitia KIA.
CHANZO:
TANZANIA DAIMA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni