Tafuta katika Blogu Hii

Jumapili, 10 Septemba 2017

ZIARA YA MGWHIRA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MAWENZI YAWA NEEMA KWA WALENGWA.




Wito umetolewa kwa watumishi wa umma katika  hospitali ya  Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (mawenzi) kuwaelimisha wananchi juu  ya haki zao katika kupata huduma stahiki ikiwemo misamaha ya uchangiaji wa gharama za matibabu kwa wazee, wajawazito na watoto.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira alipofanya ziara ya kushtukiza  katika hospitali hiyo kwa lengo la  kujionea utaratibu unaotumika  katika utoaji wa huduma hospitali hapo.
Mghwira amesema miongoni mwa changamoto alizozigundua ni pamoja na baadhi  upungufu wa vifaa tiba katika hodi ya watoto ,huduma stahiki kwa wanufaika wa misamaha ya uchangiaji wa gharama za matibabu hususani katika kupata matibabu pasipo kuchangia gharama.
Akifafanua zaidi amesema watoa huduma hao wanapaswa kutoa  kipaumbele kuokoa maisha ya watu pindi wanapofika kupata matibabu na baada ya hapo utaratibu za kupata vielelezo ili wapate misamaha.
"Kama mlengwa ameshafika hospitali akiwa na hali mbaya na amesahau kadi yake ya msamaha wa uchangiaji wa huduma asirudishwe nyumbani,juhudi za kuokoa maisha yake ziendelee pia hakikisheni mnamhudumia kwanza huku mkifanya juhudi za kupata uthibitisho wa msamaha wake." alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Wakati huohuo katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Aisha Amour ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuweka  vipeperushi na mabango ya kiada na ziada  yatakayoelekeza huduma zilizo rasmi katika utoaji wa  elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo yaliyopewa  msamaha ambapo kwa kufanya hivyo yatasaidia wanaowauguza walengwa kuyafikia malengo yaliyokusudiwa katika utoaji huduma kwa mujibu wa sheria na miongozo ya serikali.
 Amesema  ni vyema wanajamii wakafundishwa na kuelekezwa pindi wanapohitaji msaada kupitia mabango hayo na ikiwa yatachakaa yawekwe mengine mapya kadri  iwezekanavyo na kuongeza dhana yauwajibikaji kwa watumishi wa umma na kuepukana na lawama kutoka kwa wananchi katika kupata huduma kwa wakati.
Hata hivyo kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Mkoa Dk. Jonas Mcharo amekiri kutokuwepo kwa vipeperushi hivyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi hao ambapo kwa asilimi kubwa yataleta tija na kuwanufaisha wananchi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni