Swala la elimu nchini Tanzania Je?walemavu wanahaki sawa ya
kupata elimu? Haki ya
kupata elimu kwa wote ni moja ya kauli mbiu inayosadifu maendeleo ya kukua kwa
sera na mipango mkakati huru na maendeleo nchini Tanzania . Je? kuna ukweli gani inayodhihirisha
kauli hiyo kwa watu wenye ulemavu?
Watanzania wazalendo
hatuna budi kujiuliza kwa pamoja Je,
walimu wenye dhamana ya kuwafundisha
walemavu wana moyo wa upendo na watoto wenye ulemavu?
Je, vifaa
vya mafunzo na vya kufundishia vinakidhi haja na mahitaji ya watoto hao na Je? kuna fursa sawa ya ushiriki
kikamilifu kwa watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu?
Shirika lisilo la kiserikali nchini Tanzania Childreach
linatumia fursa maalum kuwajali ,kuwathamini na kusimamia ndoto za watoto
mbalimbali ikiwemo wenye ulemavu tofautitofauti juu ya haki wajibu na usawa
katika kuwapa kipau mbele katika elimu ,afya na mahitaji
stahki.
Kufuatia warsha
fupi ya kikao kilicholenga kupokea
taarifa ya tathimini ya mradi wa elimu na maendeleo kwa watu wasiosikia
(viziwi), Hii inaonekana ni dhahiri ,shairi
kwamba watu wenye ulemavu wanahitaji elimu maalumu licha ya kuwepo na upungufu
mkubwa wa walimu wa kufundisha katika shule maalumu hali inayobainishwa kama tatizo
na kikwazo kikubwa cha kufikia malengo katika kutimiza ndoto za walemavu.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha
kuwa Serikali inatoa mafunzo kwa idadi
ndogo ya walimu wa elimu maalum na kwa wakati mwingine walimu wasiopata mafunzo
haya maalum wanachukua jukumu la kutafuta mbinu zenye tija kukamilisha majukumu
hayo.
Ukosefu wa walimu unaonekana kuwa ni moja ya sababu inayochangia
umaskini uliokithiri na kusababisha
utegemezi wa misaada katika nchi yetu na hata kupelekea ukosefu wa ajira kwa watumishi
wenye ulemavu katika nafasi za juu za uongozi.
Matatizo mengi yanalikabili kundi hili kwa kuwalinganisha
watu wenye ulemavu na wale wasio na ulemavu na hata kuwakatisha tamaa kwa namna
moja au nyingine kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki na vitendea kazi .
Hii ni wazi kwamba hali ya umaskini kwa watu wenye ulemavu
inaonekana kushamiri kila kuchwapo kutokana na
kukosekana kwa miundombinu wezeshi hali inaonyesha kutengwa
,kunyanyapaliwa na kukosa haki sawa ya kupata elimu japokuwa sera ya
elimu nchini Tanzania inatoa haki sawa kwa kila mtu kupata elimu.
Kukosekana kwa haki hii kunadhihirika zaidi kutokana na idadi ndogo ya miundombinu,Taasisi ikiwemo shule zinazotoa elimu maalumu
ikilinganishwa na haja kubwa ya uhitaji wa walengwa .
Zoezi la utoaji elimu kwa wenye ulemavu wa kutosikia
linaonekana katika sera na miongozo ya
elimu kama kivuli hafifu kinachoshindwa kuonesha taswira halisia kutokana na upungufu wa vitendea kazi.
Upungufu wa vifaa hivyo wezeshi wakati mwingine unachangia kuzorota kwa msingi imara kwani
wakati mwingine katika taasisi hizi muhimu vifaa hivi vinakua havipo na kama vipo havikidhi mahitaji kwa walengwa.
Matokeo yake watu wenye ulemavu huchanganywa na wale
wanaojiweza na mara nyingi hutegemewa kushindana katika muundo mmoja wenye vigezo
vya kielimu.
Hili ni tatizo kubwa katika jamii kwa sababu panapokuwepo na
mlemavu wa kusikia anachanganywa na walemavu wengine kama wasiona na wenye mtindio
wa ubongo , kitaswira inabidi mwalimu wa wanafunzi hawa awafundiswe polepole ili waende sambamba
na wenye upeo mpana.
Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wanatoka
kwenye familia masikini kutokana na familia nyingi hushindwa kumudu baadhi ya gharama
za afya, matibabu na miundombinu wezeshi ambayo itawasaidia kundi hili
kujiajiri wenyewe na kumudu shughuli zao za kila siku.
Nchini Tanzania jamii yetu imekuwa katika hitaji kubwa la
kupata msaada wa kisheria ikiwemo kuwalinda walemavu huku baadhi ya wazazi/walezi huwachukulia walemavu kama kikwazo na watu wasioweza kushiriki katika
kupata elimu na huduma nyingine nyingi za kijamii.
Kumekuwepo na mitazamo tafautitofauti katika jamii ambapo wazazi wa
watoto hao wamekua wakiamini bila elimu
walemavu wana nafasi kubwa ya kuishi katika hali ya utajiri kwa maisha yao yote kutokana na kupata misaada
midogomidogo na kuwafanya walemavu kuwa kama sehemu ya mradi na kuwa chanzo cha
kutokupata elimu itakayo wasaidia kukabiliana na changamoto za kimaisha hasa
kiuchumi .
Wakati mwingine‘’Wazazi wana mategemeo kidogo kutoka kwa
watoto wenye ulemavu na kuwa na mitazamo kuwa watu wenye ulemavu hawawezi
kuelimishwa na muda mwingine wanawaona kama ni dhaifu na mzigo kwao hali
inayoongeza unyanyapaa zaidi katika
familia na umaskini unaochangiwa na kipato kidogo au kiwango kidogo cha elimu miongoni mwa familia na kujenga uhalisia wa imani zilizosheheni mila na dhana
potofu’’
Hali ya umasikini inachangiwa na miundo mbinu kwa walemavu
kutopata huduma sawa katika elimu ,afya na huduma nyingine kwani majengo katika
taasisi nyingi hayawaruhusu kuzifikia huduma hizo kwa urahisi mfano ngazi na
majengo ya ghorofa.
Katika hatua nyingine inayowafanya walemavu kutopata elimu
sawa kama watoto wengine hasa katika sekta ya elimu ni utaratibu wa jinsi ya
kujisajili katika shule za kata “walimu wakuu wanavyoandikisha wanafunzi kwa
njia ya kupunguza idadi yao.”
Kwa dhana hiyo watu
wenye ulemavu huachwa kwa kisingizio kwamba hakuna waalimu na vifaa kwa ajili
ya mahitaji hayo maalumu .
Inaonekana kwamba watu wenye ulemavu wanapochanganywa na
wanaojiweza wanafanyiwa mambo yasiyofaa ikiwemo kunyanyanyaswa na kunyanyapaliwa
na hatimaye kujiona kama wakati mwingine wanabaguliwa kushiriki katika shughuli nyingi zilizopo ndani ya mitaala
kama michezo na kadhalika.
Upungufu mkubwa wa
vifaa katika shule za wanafunzi wenye ulemavu
na lugha za alama ndiyo sababu kubwa inayochangia kutokuwepo kwa usawa wa elimu kwa watu wote .
Matatizo yote haya yanayowakabili watu wenye ulemavu yanachangia
kukosa usawa katika elimu na huweza kutatuliwa kwa kuwepo na wataalamu wa
kutosha na wenye sifa za kitaaluma pamoja na maslahi tofauti na waalimu
wanaofundisha wanafunzi wengine ili kuongeza hamasa na ari ya kufanya kazi kwa bidii.
Kama ilivyo katika unyanyapaa na ubaguzi kwa misingi ya
jinsia ambapo mtoto wa kiume hupewa kipaumbele zaidi kuliko wa kike hali
kadhalika mtoto mwenye viungo vyote asiye na ulemavu hupewa nafasi zaidi katika
kupata haki kuliko mlemavu hivyo mwandishi wa makala hii anabainisha baadhi ya viashiria na kukosekana kwa haki ya kupata elimu na usawa.
Kama hali hii itaendelea athari za baadae kwa kundi hili
linalo nyimwa haki ya elimu na usawa ni umaskini uliokithiri,mateso,chuki,fikra
potofu na penginepo utegemezi wa kudumu .
Serikali na mashirika ya kijamii licha ya kuendelea kutoa
huduma za ushauri na msada wa kisheria dhidi ya ukatili wadau wanahitajika
kufanya kampeni kisaikolojia kuwahamasisha wananchi kuhusiana haki,wajibu na
kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili watu wenye ulemavu ili kuendana na
sera ya taifa nchini Tanzania “serikali ya viwanda” ambapo kupitia shule hizo
wanafunzi hao wenyeulemavu wamekua wakifundishwa elimu ya ujasiriamali na
kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Mbali na kuwepo kwa harakati hizo katika kutimiza majukumu
halali kisheria kwa muktadha wa kukuza
na kutambua haki za binaadam jamii inapaswa kutambua kwamba ni watu wenye
mahitaji muhimu na ni binadamu kama wengine.
Kusimamiwa kwa sheria za haki za kibinaadam kwa ushiriki
sahihi kwa misingi imara katika taasisi muhimu
za kisiasa ,kiuchumi na kijamii zenye dhamana kubwa ya kurahisisha
huduma stahiki pamoja na kutoa kipau mbele kwa kundi hili ndio njia pekee ya ukombozi
kwa walemavu kwa kutenga fedha za ujenzi
na uboreshaji wa shule maalum kwa ajili ya walemavu na vifaa vya
kufundishia walemavu wasio ona, viziwi, bubu
pamoja na wenye utindio wa ubongo kutasaidia kundi hili kustawi na kuondoa
dhana ya unyanyapaaji.