Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ)
imesema baadhi ya vipengele katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka
2016 inakiuka uhuru wa kujieleza pia vinapingana na Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao Tanzania imeuridhia.
Mahakama hiyo imetoa hukumu dhidi ya sheria hiyo
iliyopitishwa na Bunge Novemba 2, 2016 na kusainiwa na Rais John
Magufuli hii leo.Duru za kimahama zimesema kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2017 ilifunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wakilalamikia ukandamizaji wa uhuru wa habari.
Katika hatua hiyo vipengele vilivyolalamikiwa ni 18ambapo walalamikaji wameiomba mahakama hiyo itamke kwamba vipengele hivyo vinakiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuilazimisha serikali kuvifuta kabisa.
Hukumu hiyo imesomwa leo Alhamisi Machi 28, mbele ya Jopo la majaji watatu Jaji Charles Nyachae, Monica Mugenyi na Jaji Justice Ngie.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Nyachae amesema vifungu vilivyo kwenye sheria hiyo ni vibovu na vinavyokiuka mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ameitaka Serikali ya Tanzania kurekebisha vifungu vya Sheria ya Uhuru wa Habari kutokana na kukiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
"Sheria hii inapaswa kufanyiwa marekebisho ili iendane na mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya," amesema Jaji Nyachae.
Wadai halo walikua wakitetewa na mawakili, Fulgence Massawe, Jebra Kambole, Mpale Mpoki , Donald Deya na Jenerali Ulimwengu.
Mahakama hiyo imekubaliana na walalamikaji kuwa vifungu katika sheria ya Huduma ya Habari vya (3)(a), 13, 1920, 21,34 pamoja na vifungu vingine vinakiuka utawala bora, demokrasia na utawala unaozingatia sheria na inapingana na mkataba ulioanzisha EAC.
Hata hivyo Wakili kiongozi wa walalamikaji, Fulgence Massawe amesema ushindi huo ni wa kihistoria na unathibitisha hoja za wadau mbalimbali walizokua wakisema sheria hiyo siyo nzuri kwa maslahi mapana ya nchi.