Serikali
mkoani Kilimanjaro imezindua kituo maalum cha kuuzia madini ya Vito katika
wilaya ya Same kitakachosaidia kuleta tija kiuchumi na kuzuia utoroshaji wa madini unaofanywa na baadhi ya wachimbaji
wadogo wadogo wilayani humo na wafanyabiashara
wa mikoa jirani.
Mkuu wa
mkoa huo, Dk. Anna Mghwira amebainisha
hayo katika ziara yake ya kikazi ya siku moja iliyolenga kujioneo sampuli mbalimbali za
madini hayo sambamba na kukizindua
chumba rasmini kitakachotumika kufanyia biashara hiyo kwa muda wakati tafiti za
kina zikiendelea .
Akizungumzia
swala hilo nyeti mkuu huyo amesema Wilaya ya Same ni miongoni mwa wilaya nne
zinazopatikana madini ya vito ikiwemo wilaya ya Mwanga ,Rombo na Siha.
Dk.
Mghwira amesema madini mbalimbali ya Vito pamoja na madini ya ujenzi yanayopatikana
mkoani humo yamekua yakisafirishwa na kupelekwa nje ya mkoa huo kwa matumizi
tofautitofauti ya viwandani kwa njia
zisizo halali .
“Wilaya
hii inapatikana madini mbalimbali kama vito , madini ya ujenzi na madini ya
viwandani ambapo wapo wachimbaji wamekuwa wakiyatorosha na kwenda kuyauza nje
ya mkoa wetu hivyo kuwepo kwa kituo hicho kutadhibiti biashara hiyo” amesema
Dk. Mghwira.
Akifafanua
zaidi Dkt.Mgwhira amesema, kituo hicho cha kuuzia madini kitakuwa maalum kwa
ajili ya kuuzia madini ya vito yanatopatikana kwa asilimia kubwa katika ukanda wa milimani ambapo yataibua fursa
za ajira kwa wazawa kama ilivyo azima ya Serikali kuwahudumia wananchi wake na kupanua wigo katika sekta ya viwanda kwa kuzingatia rasilimali ghafi
zilizopo .
Mkuu huyo amesema,
uwepo wa kituo hicho cha kuuzia madini kutaamsha hari hamasa kwa wazawa kuwekeza katika sekta hiyo
kisheria ikiwemo kujisajili na kupata leseni itakayowawezesha kufanya biashara hiyo kwa halali ikiwa ni
pamoja na kulipa kodi stahiki ya Serikali.
”Tumekua
tukipata hasara pasipo kujua umuhimu wa rasilimali zetu hivyo sisi kama watendaji inatubidi tuwe macho
na kutumia fursa zilizopo kukuza uchumi kwa maslahi ya taifa kwa kuweka mbele
uzalendo ,utashi na uwajibikaji bado serikali inaendelea na mchakato ili kuona
umuhimu wa kuanzisha kituo kingine kwa ajili ya kuuzia madini ya ujenzi ya viwandani”amesema Mgwhira .
Akizitaja fursa
zilizopo katika wilaya ya Mwanga amesema kunapatikana madini ya Shaba, Vito na
madini ya ujenzi, wilaya ya Rombo yanapatikana madini ya Pozolana na matofali ya kuchonga
ambapo huuzwa nchini Kenya kwa wingi huku wilaya ya Siha kukipatikana madini ya
Ujenzi.
Kwa upande
mkuu wa wilaya ya Same, Rosemary Senyamule amesema , kufunguliwa kwa kituo
hicho kutasaidia kukuza uchumi wa wilaya ya Same na mkoa wa Kilimanjaro kwa
ujumla na kukidhi mahitaji ya ziada na kiada kupitia huduma mbalimbali za
kijamii ikiwemo afya,elimu,miundombinu stahiki.
Katika
hatua hiyo Senyamule ametumia nafasi hiyo kuwataka wachimbaji wadogo wilayani humo
kuchangamkia fursa hiyo kwa kukata
leseni za uchimbaji wa madini hayo ya vito ili kuepuka migogoro mbalimbali isiyo na tija hapo baadae.
Aidha
ametoa onyo kwa wachimbaji na wafanyabiashara wialayani humo kuacha mara moja
tabia ya kutorosha madini na badala yake wafike katika kituo hicho cha kuuzia
madini ili serikali iweze kukusanya kodi stahiki kwa maendeleo ya Taifa.